Katika Maisha ya kila siku..
Kwa chochote kile unachokifanya iwe biashara, uandishi au mpiganaji wa masumbwi ili uweze kufanikiwa kwa viwango vya juu sana, ni wazi kabisa unahitaji kujijengea tabia ya kuwa na umakini.
Tatizo la watu wengi hawapo makini sana katika mambo yao au mfumo mzima wa kuendesha maisha yao.
Kama vile madereva wa magari walivyo makini wawapo barabarani, vivyo hivyo nawe unatakiwa kuwa makini sana kwenye maisha yako.
Umkini wako ndio utakaokupa mafanikio
Hebu piga picha kama dereva wa gari asipokuwa makini awapo barabarani ni nini ambacho huwa kinatokea?
Bila shaka hakuna jibu jingine ambalo utanipa zaidi ya ajali.
Hata kwenye maisha yetu hivyo ndivyo tunavyosababisha ‘ajali’ za kushindwa sana wakati mwingine kwa sababu ya kupoteza ule umakini.
Unatakiwa kujiwekea umakini katika kila eneo la maisha yako ili ufanikiwe.
Na ili uwe makini yapo mambo kadhaa mbayo unatakiwa kuyafanya na kuyazingatia sana kila siku kwenye safari yako ya mafanikio. Unaposhindwa kuzingatia mambo hayo, ni lazima umakini utapotea na utaanza kuishi maisha ya kushindwa.
1. Anza siku yako upya.
Haijalishi jana yako ilikuwaje, kilicho kikubwa kwako ni kuanza siku yako upya. Sahau changamoto zote ulizokutana nazo jana ambazo pengine zilikukatisha tamaa sana.
Kitu cha msingi kwako anza siku yako upya kwa kuzingatia kile unachotaka kukifanya. Ikiwa utakuwa unazingatia sana mambo ya jana, hapa ni lazima umakini utakutoka na utashindwa kufanikiwa.
2. Andika malengo yako ya siku.
Acha kuishi kiholela, ishi kwa mipango kwa kuandika malengo yako ya siku, Hiyo itakusaidia kukuongezea umakini na kujua hasa ni kipi ufanye au kipi usiweze kufanya.
3. Tumia muda wako vizuri.
Matumizi mazuri ya muda ni chanzo kingine kikubwa cha kukusaidia kuweza kuwa makini. Kama unatumia muda wako hovyo, ni wazi au dalili ya wewe kutokuwa makini,
zingatia sana matumizi yako ya muda.
4. Jiwekee mipango yako ya mbele.
Unapokuwa na mipango yako ya mbeleni uliyojiwekea, kwa mfano kujua ni nini utakifanya mwezi ujao au mwaka kesho, hiyo inasaidia sana kuongeza nguvu ya umakini kwa kile unachokifanya.
Naomba utambue kwamba siri nyingine ya mafanikio yako ipo kwenye umakini ulionao. Umakini ulionao ndio unaonyesha kwamba upo na nia ya kufikia kwenye mafanikio yako.
Hata hivyo kumbuka huwezi kuwa makini mpaka ujijengee tabia ya kuanza siku yako upya,
kutumia muda wako vizuri,
kuandika malengo kila siku na kujiwekea mipango ya mbeleni.
Ukizingatia hayo kwenye maisha yako basi kukata tamaa ya maisha itakuwa mwiko.
No comments:
Post a Comment